Kama Bado Hujajiunga Nami, Unaweza Kujiunga Kwa Kubonyeza Like Hapa Chini Nikutumie Habari Moja Kwa Moja
Hatua hiyo imekuja baada ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inayoongozwa Ukawa kuzuia Sh. 5 bilioni, fedha mali ya Kampuni ya Simon Group Limited.
Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na Ridhwan Kikwete, mtoto wa rais huyo na Prof. Juma Kapuya, aliyekuwa Mbunge wa Urambo Magharibi wanatajwa kuwa miongoni mwa wana hisa kwenye shirika hilo.
Simon Group Limited ililipa fedha hizo kwa halmashauri hiyo ikiwa ni sehemu ya malipo ya ununuzi wa hisa za UDA.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Saed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo amesema halmashauri haikuuza UDA licha ya Simon Group Limited kudai kununua.
Kwenye mkutano huo ambao pia uliohudhuriwa naIsaya Mwita Charles, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Kubenea amesema, mkutano uliokabidha UDA kwa Simon Group uliitishwa bila baraka za wenye mali – Baraza la Madiwani la Jiji na Msajili wa Hazina na kwamba, ulihudhuriwa na watu wanne tu.
“Kwanza tunataka mtambue halmashauri haikuuza UDA kwa kuwa, Simon Group Limited wametumia hati ya UDA – mali ya wananchi kufanya biashara. Haturudishi fedha hizi mpaka tufanye hesabu, tujue kampuni hii imepata faida kiasi gani.
“Hata katika mradi wenyewe wa UDA-TR, kumesheheni utapeli. Unaoitwa mkutano mkuu maalum wa wana-hisa wa tarehe 10 Juni 2011, uliosimamiwa na Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji kuidhinisha pamoja na mengine, uuzaji wa hisa za UDA, haukuwa halali,” amesema Kubenea.
Kubenea amesema, mkutano uliokabidha UDA kwa Simon Group uliitishwa bila baraka za wenye mali – Baraza la Madiwani la Jiji na Msajili wa Hazina na kwamba, ulihudhuriwa na watu wanne tu
“Watu hawa ni Dk. Didas Masaburi mwenyewe ambaye alikuwa mwenyekiti; Mkurugenzi wa Simon Group, Robert Kisena ambaye alikuwa katibu; Mwanasheria wa jiji, Isaac Nassor Tasinga na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Phillip Mwakyusa,” amesema Kubenea.
Amesema, kwenye mkutano huo Masaburi alitangaza Kampuni ya Simon kuwa ‘imetimiza masharti yote ya mkataba wa kupewa hisa, mali na uendeshaji wa UDA.’
Ameeleza kuwa, mwaka 1983, Msajili wa Hazina alitoa asilimia 51 ya hisa na kuipa Halmashauri ya Jiji huku Serikali Kuu ikibakiwa na asilimia 49 na kwamba, shirika hili liliwekwa katika orodha ya mashirika ya kurekebishwa na serikali mwaka 1997.
“Taarifa ya serikali ya tarehe 3 Agosti 2011 kwenda Kamati ya Bunge ya Miundombinu inaeleza mkutano huo ulikuwa batili kwa kuwa, ulikiuka Katiba ya UDA, kifungu namba 45 kutokana na kutotimia kwa akidi na kukosekana kwa msajili wa hazina,” amesema Kubenea.
Taarifa hiyo imeeleza, kikao hicho hakikuwa na mamlaka ya kufanya uamuzi, na kuwa maazimio yote yaliyofikiwa yalikuwa batili.
“Kwa taarifa hii pekee, serikali ilipaswa kuiondoa Simon Group kwenye uendeshaji wa UDA ikiwemo kukodishwa mali zake, hadi hapo uchunguzi wa suala hilo utakapokamilika. Haikufanya hivyo,” amesema Kubenea.
Kubenea amesema, kwa taarifa hiyo pekee ilitosha serikali kuchunguza na kuwachukulia hatua wote waliohusika, hasa kwa kuzingatia kuwa, kabla ya kikao hicho, tayari Masaburi alishapokea barua ya tarehe 28 Februari 2011 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliyomuagiza kusitisha mara moja mchakato wa kuuza hisa za serikali ambazo hazijagawiwa.
Akinukuu barua kutoka kwa Waziri Mkuu yenye Kumbukumbo Na. 185/295/01/27, amesema Masaburi na wenzake waliendesha mkutano huo wakiwa na kabrasha la Katiba ya UDA ambayo vipengele vyake vilikuwa vinakataza walichokifanya.
“Kipengele cha 2.0 cha mkataba kinaeleza mauzo ya hisa 7,880,303 ambazo hazijagawanywa ambapo kwa majibu wa kipengele cha 2.2, mnunuzi alipaswa kulipa kwa awamu kiasi cha Sh. 1.1 bilioni,” amesema.
Aidha, anasema malipo ya kwanza ya Sh. 285. 6 milioni sawa na asilimia 25 ya malipo yalipaswa kufanywa katika kipindi cha siku zisizozidi 14 tangu mkataba kufungwa.
Lakini Simon Group haikulipa kiasi kamili kwa mujibu wa mkataba na hata kiasi ilichotoa ilikilipa nje ya siku zilizotajwa na mkataba.
KUPATA HABARI NA MATUKIO YA KILA SIKU, BONYEZA Like HAPA CHINI
Asante! TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment